MILLEN MAGESE ACHANGIA MILIONI KUMI NA TANO KWA AJILI YA UJENZI NA MADAWATI YA SHULE MJINI MTWARA.. MWANAMITINDO mahiri wa kimataifa ambae pia aliwahi kuwa Miss Tanzania 2001, Millen Happiness Magese amewagusa wakazi wa Mtwara kufuatia ziara yake ya kimafanikio aliyoifanya mkoani humo na kukabidhi misaada mbalimbali.
Millen ambae kwa sasa anaishi nchini Marekani akijishughulisha na fani ya mitindo akiwa Mtwara alipokelewa na viongozi mbalimbali wakiwamo Mkuu wa Wilaya ya Mtwara; Mhe. Willman Ndile, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara; Mhe. Simbakali na Mbunge wa Mtwara mjini; Mhe. Hasnain Murji.
Millen alitoa fedha taslim kiasi cha shilingi milioni 15 ambapo milioni 10 ilikuwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi ya Mjimwema baada ya kutembelea shule hiyo na kuguswa na hali ya mazingira magumu aliyoyakuta katika shule hiyo iliyopo kata ya Magengeni.
Millen awali alikuwa ametaka kupeleka msaada wake huo katika shule ya msingi ya LiLilungu iliyopo Mtwara mjini lakini alijikuta akimwaga milioni kumi kwa shule ya Mjimwema na kuongeza milioni tano kwa ajili ya madawati ya shule ya Lililungu kwani awali alikuwa ameahidi kutoa milioni kumi.
Shule hiyo yenye madarasa mawili yaliyojengwa kwa udongo ambapo wanafunzi wakiwa ni wengi huku wengi wao wakiwa hawana viatu na sare zao za shule zikiwa zimechakaa.
Akizungumza shuleni hapo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Ndile, Millen alisema kuwa akiwa kama mwanamitindo ameguswa na hali mbaya ya mazingira ya shuleni hapo hasa ikizingatiwa kuwa wanafunzi wanasomea katika shule ya udongo huku wakiwa na mazingira duni ya kufundishia.
 Millen Magese akipokelewa na Mheshimiwa Ndile pamoja na Afisa Elimu manispaa ya Mtwara, Mama Florah Aloys
Aliongeza na kusema, "Mwaka 2001/2002 nilitembelea mkoa wa mtwara ambao ulinigusa sana kwenye swala zima la elimu haswa mazingira ambayo yanamfanya mtoto akae chini. Na nikaahidi siku moja mungu akijalia nitarudi Mtwara na nimesikitika ni miaka 12 sasa bado watoto wanakaa chini nikaone nirudi kutimiza ahadi na kutoa hamasa kwenye swala hili la elimu Mkoani mtwara”; mbali na milioni kumi na tano pia aliahidi kuwatafutia sare za shule wanafunzi hao jozi mbili kila mmoja na pia alikubali kuwa mlezi wa shule hiyo.
Millen Magese akipokelewa na mkuu wa Mkoa Mtwara , Mhe. Simbakalia, pembeni yake ni Mbunge wa Mtwara, Mhe. Hasnain Murji  
Pia alipata fursa ya kukaa na wajasiriamali walioandaliwa semina na mkuu wa wilaya pamoja na mbunge wa Mtwara mjini kujadili mbinu za kuwaongezea kipato na kwa kuanzania milioni sita iliyopatikana iligawanywa kwa wajasiriamali kulingana na vikundi ili wao watengeneze madawati kwa ajili ya watoto wao, ambapo milioni tano ilitolewa na Millen Foundation na milioni moja ilitolewa na Mhe. Murji
Naye mkurugenzi wa manispaa alisema Millen ameweka historia kwani kitu hiki hakijawahi kufanyika Mtwara na mtu binafsi wanaangalia ni jinsi gani Millen Magese atakumbukwa kama muanzilishi wa ujenzi wa shule ya mji mwema.

Millen Magese akikabidhi hundi ya milioni kumi na tano kwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Mhe. Wilman Ndile; kulia ni Mbunge wa Mtwara Mjini, Mhe. Hasnain Murji


 Millen Magese akisaini kitabu cha wageni ofisini kwa mkuu wa wilaya Mtwara kabla ya kuanza ziara ya kutembelea mashuleni.
Baada ya kuzungumzia ahadi yake hiyo Millen aliwahamasisha wadau wengine aliiongozana nao kuchangia mchango wa shule hiyo akiwamo Mbunge wa Mtwara mjini Murji ambae aliahidi kutoa mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kufanikisha ujenzi zaidi wa shule hiyo na shilingi milioni moja kwa ajili ya madawati.
 Naye Mkuu wa Wilaya ya Mtwara; Mhe Ndile pamoja na Mhe. Murji waliwataka wananchi kuhamasika zaidi kwa kuunga mkono harakati za Millen katika kuimarisha elimu mkoani humo kwa kuwa ameonesha mfano mzuri akiwa kama mwanamitindo.
Mwisho

No comments: